SABABU 8 ZA NDOA KUFELI Unapoingia katika ndoa, huwezi kufikiria hata kidogo kwamba asilimia kubwa ya ndoa hufeli. Ndoa zinaweza kufeli...
SABABU 8 ZA NDOA KUFELI
Unapoingia katika ndoa, huwezi kufikiria
hata kidogo kwamba asilimia kubwa ya
ndoa hufeli. Ndoa zinaweza kufeli kwa
sababu nyingi na iwapo ndoa yako
ilianguka na kufeli sababu kubwa yaweza
kuwa na tofauti nyingine nyingi. Lakini,
kuna sababu kadhaa za jumla na za
kudumu kwenye ndoa zote zilizofeli.
Hebu tazama orodha yangu ya sababu 8
za ndoa nyingi kuanguka na kufeli.
1) Kwa sababu ulitaka harusi badala ya
ndoa:
Ni miongoni mwa ada za kijamii kushiriki
katika furaha mbalimbali za wenzetu.
Miongoni mwa furaha hizo ni shughuli za
harusi pindi wahusika wanapoamua
kuingia katika taasisi tukufu ya NDOA.
Shamshamra zinazoandamana na tukio
hilo adhimu hutuhamasisha kuingia katika
taasisi hiyo muhimu kabisa katika maisha
ya mwanadamu. Mavazi, mapambo ya
maharusi na kushangiliwa na wenzetu
huwafanya wanandoa wahisi kama nyota.
Matukio hayo hukufanya uanze kutamani
na hata kupanga namna harusi yako
itakavyokuwa. Tazama: hapo
umesukumwa na mvuto wa harusi badala
ya uhalisia wa NDOA. Ni bahati mbaya
kuwa maandalizi ya harusi yanakuwa
makubwa kuliko hata maandalizi ya NDOA
yenyewe. Nawashauri wazazi kuwashauri
watoto wao kwamba: baada ya harusi
kuna ndoa. Hivyo nguvu kubwa
wazielekeze kwenye suala la pili.
2) Kwa sababu umeoana na mtu
usiyeendana naye:
Wakati fulani jambo hili hutokana moja
kwa moja na suala la kwanza nililolieleza
hapo juu, lakini kuna sababu nyingine
ambazo zinaweza kusababisha kufunga
ndoa na mtu ambaye hamuendani kabisa.
Yumkini ni mtu uliyemzoea; yumkini ni
mtu uliyecheza naye tokea utotoni lakini
licha ya kutokuwa mtu sahihi unajisemea
moyoni na kujipa matumaini “siwezi
kuuvunja moyo wake… mambo
yatabadilika tu”. Yumkini unaona kabisa
amekuwa tofauti na ulivyotarajia, lakini
umeshaweka ahadi naye. Kabla ya kuingia
katika ndoa jitahidi umjue vilivyo mwenza
wako wa maisha…. Usiangalie tu kwamba
atapendeza ukisimama naye siku ya
harusi.
3) Kwa sababu mtu mmoja hawezi kukidhi
mahitaji yako yote:
Jambo hili ni miongoni mwa sababu kuu
za ndoa nyingi kufeli na hata kuanguka.
Tatizo ni kwamba hata kama mwenza
wako anakidhi asilimia 75 ya mahitaji yako
makubwa kabisa kila siku, asilimia
nyingine 25 haitatimizwa moja kwa moja.
Hivyo, kwa mfano ukiolewa na
mwanaume mchapakazi, mwenye mvuto
na anayekupa raha kitandani, lakini
hakuiti kwa majina mazuri yenye
kukupendeza na hakusikilizi, unatakiwa
kujifunza kuridhika na hiyo asilimia 75,
kwa sababu hakuna anayeweza kukidhi
mahitaji yako kwa asilimia zote. Wengine
huwa wanashindwa kiasi kwamba
wanafikia hatua ya kutafuta sehemu
wanayoweza kujaza hizo asilimia 25
wanazozikosa. Hata huko wanakokwenda
hawawezi kupata mtu anayeweza kuwapa
furaha kwa asilimia zote na hujikuta
wakiingia katika matatizo makubwa zaidi.
4) Kwa sababu ya usaliti:
Baadhi ya watu baada ya kukosa baadhi ya
mambo machache kutoka kwa wenzao,
kama nilivyosema katika namba 3, hukosa
kuridhika na hivyo kuanza kutafuta mahali
wanapoweza kukidhi ombwe hilo. Yumkini
ukawa na hitajio la jambo dogo lakini
kumbe hata huko ukawa huwezi kulipata.
Yumkini ulihitaji tendo la ndoa lakini
yumkini hitajia lako halisi ni zaidi ya hilo.
Usaliti ni jambo la hatari sana kwenye
ndoa yoyote, na likishatokea basi mambo
hayawezi kuendelea kuwa katika hali ya
kawaida. Mara nyingi pigo hilo huipeleka
ndoa kwenye maporomoko.
5) Kwa sababu umekata tamaa mapema:
Sio kila tatizo huvunja uhusiano. Ni
kawaida kwa wanandoa kukutana na
mambo mazito katika maisha yao.
Hukutana na matatizo ya kiuchumi, kufiwa
na watoto na hata kutukanwa… lakini
bado huendelea kuwa imara na kuwa
pamoja na hakuna anayemkimbia
mwenzake. Kuna wengine wanapokutana
na matatizo mazito hukata tamaa
mapema, huhisi kuwa hawawezi kufanya
stahmala… hudhani kuwa changamoto
hizo hawatozipata wakienda sehemu
nyingine.
6) Kwa sababu hakuna fedheha:
Katika miaka ya 1800, kiwango cha talaka
kilikuwa kidogo mno. Mwaka 1915 katika
baadhi ya maeneo ndoa ilikuwa asilimia 5
ya ndoa zote, na ilikuwa kwa matukio
maalumu kama vile unyanyasaji, uzinifu
au utelekezaji wa familia.
Katika baadhi ya maeneo, ili watu
kuachana walihitaji kuidhiniwa na viongozi
wa kiroho, wazazi na hata jamii za
wahusika. Hata hivyo, wanandoa wengi
walipata changamoto kubwa sana kwa
sababu walilazimika kuishi katika ndoa
zenye machafuko kwa sababu
wasingeweza kustahmili “aibu” ya talaka.
Suala la talaka lilionekana kama ni
fedheha na aibua katika jamii. Lakini leo
hii suala la talaka limekuwa jambo la
kawaida na ni rahisi kufanywa na
kukubaliwa na jamii. Watu wengi hawajali
gharama zinazotokana na kuachana.
7) Kwa sababu unadhani kuwa wengine
ndio wanaokosea:
Kuna kasumba mbaya sana katika baadhi
ya ndoa ambapo mtu mmoja huwa
MKAMILIFU na mwingine huwa
MKOSEFU. Mwanandoa mmoja anaweza
kujiona kuwa yeye hakosei na kumuona
kuwa mwenza wake ndiye mkosefu siku
zote. Hili ni tatizo ambalo huzigharimu
ndoa nyingi. Ni muhimu sana kama
wanandoa watakuwa watu SAHIHI badala
ya kuwa WAKAMILIFU. Kwa sababu hilo ni
jambo lisilowezekana. (Rejea mada yangu
ya KANUNI YA SEKUNDE 30).
8) Kwa sababu wewe unataka upendo
wakati yeye anahitaji heshima:
Jambo la kawaida, lakini ndoa hufeli pindi
wanandoa wanaposhindwa kulielewa. Kwa
ujumla mke ana silika ya kuhitaji upendo,
ilhali mume anahitaji vipawa vyake
vitambuliwe na kuheshimiwa. Tatizo ni
kwamba tunajaribu kuwapa wenza wetu
mambo ambayo tunayataka sisi, sio yale
yanayoendana na silika zao. Angalia kwa
mfano mke anamkosoa mume wake
mbele ya watoto, mbele ya watu au hata
kumuandika vibaya katika mitandao ya
kijamii, hakika hilo litamvunjia heshima
mume. Angalia pia mume ambaye
anayejigamba kwa wengine kuhusu
mkewe lakini akiwa nyumbani
anampuuza. Ewe mume onesha upendo
kwa mkeo, ewe mke mheshimu mumeo,
mtaona mabadiliko
COMMENTS